TRANSLATE THIS BLOG

Monday, January 7, 2013

YADAIWA FERGIE ANASAKA KIPA MPYA!!

WALENGWA NI BEGOVIC & REINA!

GAZETI la Uingereza, The Mirror, limeripoti kuwa Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson anafikiria kumpiga shoka David De Gea na kusaka Kipa mpya katika kipindi hiki cha Dirisha la Uhamisho la Mwezi Januari.

Gazeti hilo limedai Sir Alex Ferguson amezidi kuvunjwa moyo na uchezaji wa Kipa De Gea ambae anashindwa kudhibiti eneo la Penati Boksi na mara nyingi huonekana mwenye mchecheto katika eneo hilo, hasa kwa mipira ya juu ya frikiki na kona, ambayo wapinzani wamechukulia hilo kama ni udhaifu wa Manchester United.

 The Mirror limedai kuwa Ferguson amemwomba Mkurugenzi Mtendaji, David Gill, pamoja na Wamiliki wa Klabu, Familia ya Glazers, kutoa Fedha ili kumnunua Kipa ambae ataruhusiwa kuichezea Man United kwenye Mashindano ya UEFA CHAMPIONZ LIGI Msimu huu.

Tangu atue Man United kutokea Atletico Madrid Mwaka 2011, De Gea amekuwa hana namba ya kudumu na mara nyingi amekuwa akibadilishana na Kipa mwingine, Anders Lindegaard, kutoka Denmark.

Ripoti za Gazeti hilo zimedai walengwa wa Sir Alex Ferguson ni Makipa wa Stoke City, Asmir Begovic, na yule wa Liverpool, Pepe Reina, kwani wote wataruhusiwa kuichezea Man United kwenye Mashindano ya UEFA CHAMPIONZ LIGI.

Hata hivyo, kumng’oa Begovic kutoka Stoke City itakuwa kazi kubwa kwani yeye ndie moja ya nguzo kubwa Klabuni hapo lakini duru hizo za habari zimekiri kumpata Reina ni rahisi kidogo maana inaonekana sasa Liverpool inatafuta mwelekeo mwingine kuhusu Kipa.

No comments:

Post a Comment