TRANSLATE THIS BLOG

Friday, November 16, 2012


Papiss Cisse hatihati kuikosa Newcastle v Swansea...

Bosi wa Newcastle Alan Pardew ametoboa kuwa Papiss Cisse huenda asicheze Mechi ya Ligi Kuu Jumamosi dhidi ya Swansea kwa sababu ya mgogoro na Senegal kufuatia Straika huyo kutojiunga na Timu ya Taifa ya Senegal ambayo Jumatano, Siku ya Kalenda ya FIFA, ilicheza Mechi ya Kirafiki na Niger.

Inadaiwa sasa Senegal wametishia kuitumia Sheria ya FIFA ya kumfungia Papiss Cisse kwa Siku 5 kwa sababu hawakujulishwa kuhusu Mchezaji huyo kutojiunga na Timu ya Taifa.


Pardew amedai Cisse alikuwa na maumivu ya mgongo aliyoyapata kwenye Mechi ya Jumapili iliyopita waliyofungwa 1-0 na West Ham ambayo yalimlazimu Mchezaji huyo kutolewa nje kwenye Mechi hiyo.

Newcastle imedai ilituma Ripoti ya Madaktari kuhusu Cisse kwa Barua Pepe kwa Chama cha Soka cha Senegal lakini Pardew amesema inaelekea haikupokelewa.

Ikiwa Cisse, Miaka 27, ataikosa Mechi na Swansea hilo litakuwa pigo kwa Newcastle ambao wanahitaji ushindi kwa vile wameshinda Mechi moja tu kati ya sita zilizopita za kwenye Ligi.

Pardew amesema kuwa wanawasiliana na FA ya England na Viongozi wa Senegal ili kupata uhakika kama wanaweza kumtumia Mchezaji huyo Jumamosi.

Luis Suarez ni furaha kubakia Liverpool Miaka mingi!!

Straika wa Liverpool Luis Suarez amesema anafurahia kubakia Liverpool na anataka awe hapo kwa Miaka mingi ingawa sasa kuna tetesi kubwa Manchester City wanataka kumsaini Mwezi Januari Dirisha la Uhamisho likifunguliwa.


Mwanzoni mwa Msimu huu, Suarez alisaini Mkataba mpya na Liverpool na Msimu huu amekuwa kwenye fomu nzuri kwa kufunga Mabao 11 katika Mechi 16 alizochezea Liverpool.

++++++++++++++++++++++++++
Luis Suarez akiwa Liverpool
-ALISAINIWA: Januari 2011 (£22.7m)
-MECHI: 68
-MAGOLI: 32
++++++++++++++++++++++++++

Hata hivyo, Meneja wa Liverpool, Brendan Rodgers, amesema Mchezaji huyo hauzwi.

Rodgers ametamka: “Tukimpoteza Suarez hatuna Straika, hivyo hatuwezi kumuuza.”

Tangu atue England Suarez, licha ya kufanya vizuri akiwa na Liverpool, amekuwa akikumbwa na migogoro ya mara kwa mara.

Alifungiwa Mechi 8 baada ya kumkashifu Kibaguzi Beki wa Manchester United Patrice Evra na baada ya hapo akazua mzozo mpya baada ya kukataa kumpa mkono Evra Timu za Liverpool na Man United zilipokutana Old Trafford.

Hata hivyo, Msimu huu, Wachezaji hao walipeana mikono Timu zao zilipokutana.

Hivi karibuni aliandamwa kwa madai kuwa hujiangusha makusudi kwenye Eneo la Penati ili kuwahadaa Marefa apewe Penati tabia ambayo wakati mwingine imemdhuru mwenyewe kwa kunyimwa Penati za wazi huku Marefa wakidhani anawadaa.

------------------------------------------------------------

No comments:

Post a Comment