TRANSLATE THIS BLOG

Friday, October 5, 2012


VPL: Ligi Kuu VODACOM kuendelea Wikiendi!

MISRI YAJITOA, Serengeti Boys kumvaa Mshindi Zimbabwe v Congo Brazaville!
KAMATI ya UCHAGUZI TFF yatoa UAMUZI!!

Ligi Kuu Vodacom itaendelea Jumamosi na Jumapili kwa Timu zote 14 kushuka Viwanjani na ifuatayo ni Ratiba kamili:

VPL: LIGI KUU VODACOM
RATIBA:
Jumamosi Oktoba 6

African Lyon v Azam [Azam Complex, Dar es Salaam]

Ruvu Shooting v Coastal Union [Mabatini, Mlandizi, Pwani]

Jumapili Oktoba 7

Simba v Oljoro JKT [Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam]

Kagera Sugar v Yanga (Uwanja wa Kaitaba, Bukoba)

Mgambo Shooting v Polisi Morogoro (Uwanja wa Mkwakwani,Tanga)

Toto Africans v JKT Ruvu (Uwanja wa Kirumba, Mwanza)

Tanzania Prisons v Mtibwa Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya)


ZIFUATAZO NI TAARIFA KAMILI TOKA TFF:

Release No. 162

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Oktoba 5, 2012

MISRI NAYO YAIKACHA SERENGETI BOYS

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) imefuzu kucheza raundi ya tatu na ya mwisho kwenye michuano ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Vijana baada ya Misri kujitoa.

Serengeti Boys ilikuwa icheze raundi ya pili dhidi ya Misri; mchezo wa kwanza ukichezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam na ule wa marudiano wiki mbili baadaye jijini Cairo.

Katika raundi ya kwanza Serengeti Boys inayofundishwa na Jakob Michelsen kutoka Denmark ilikuwa icheze na Kenya mwezi uliopita, lakini nchi hiyo ilijitoa katika michuano hiyo ambayo fainali zake zitachezwa Machi mwakani nchini Morocco.

Serengeti Boys sasa itacheza raundi ya tatu kwa kumkabili mshindi wa mechi kati ya Zimbabwe na Congo Brazzaville. Mechi ya kwanza itachezwa Novemba 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itafanyika ugenini wiki mbili baadaye.

Zimbabwe na Congo Brazzaville zitapambana zitapambana kati ya Oktoba 12-14 mwaka huu, Zimbabwe ikiwa mwenyeji wa mechi ya kwanza wakati ya marudiano itafanyika kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.

LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA SITA

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwan wa Tanzania Bara inaingia raundi ya sita wikiendi hii kwa mechi saba. Kesho (Oktoba 6 mwaka huu) African Lyon itakuwa mwenyeji wa Azam katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Nayo Ruvu Shooting itaikaribisha Coastal Union ya Tanga katika mechi itakayochezeshwa na Oden Mbaga wa Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani. Mbaga atasaidiwa na Samuel Mpenzu, Ferdinand Chacha na Andrew Shamba.

Jumapili (Oktoba 7 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Simba na Oljoro JKT itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kagera Sugar na Yanga (Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba), Mgambo Shooting na Polisi Morogoro (Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga), Toto Africans na JKT Ruvu (Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza) na Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Release No. 162b
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 5, 2012

1.           Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika tarehe 03-04 Oktoba 2012 ilijadili michakato ya chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa ya Rukwa (RUREFA), Arusha (ARFA), Shinyanga (SHIREFA), Pwani (COREFA), Dar es Salaam (DRFA) na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT). Kamati iliamua yafuatayo:

(a)        Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA)

Uchaguzi wa ARFA utafanyika  Jumapili, tarehe 07 Oktoba  2012 mjini Arusha kama ulivyopangwa.

(b)        Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT)

Uchaguzi wa FRAT utafanyika Jumapili, tarehe 07 Oktoba 2012 mjini Dodoma kama ulivyopangwa.

(c)        Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA)

Uchaguzi wa COREFA utafanyika  Jumapili, tarehe 14 Oktoba  2012 Wilayani Mafia kama ulivyopangwa.

(d)        Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA)

Kamati ilibaini na kujiridhisha kuwa kulikuwa na udanganyifu uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya RUREFA katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba hususan, uteuzi wa baadhi ya  wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA. Pamoja udanganyifu huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejiridhisha kuwa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA imeshindwa kutimiza wajibu wake katika kusimamia uchaguzi wa RUREFA, hata baada ya kuwa imepewa onyo kuzingatia matakwa ya Kanuni za Uchaguzi.

Kutokana na udanganyifu uliofanyika katika uteuzi wa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26(2) na (3) na Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), imeamua yafuatayo:

(i)  Imeifuta Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA. TFF itateua Kamati mpya ya Uchaguzi ya RUREFA itakayoandaa na kusimamia uchaguzi wa RUREFA.

(ii)Uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya RUREFA utafanyika wakati muafaka baada ya TFF kukamilisha taratibu za uteuzi, na ratiba ya uchaguzi ya RUREFA itatangazwa baada ya zoezi hilo.

(e)        Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA)

Kamati ya Uchaguzi ya TFF imebaini kuwa baadhi ya viongozi wa Kamati ya Utendaji ya SHIREFA wanaingilia mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA kinyume na matakwa ya Kanuni za Uchaguzi  za wanachama wa TFF. TFF haitambui maamuzi ya uongozi wa SHIREFA wa kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA inayosimamia uchaguzi wa Chama hicho. Zoezi la uchaguzi wa SHIREFA lililoanza tarehe 08 Septemba 2012 linaendelea na uchaguzi wa viongozi wa SHIREFA utafanyika tarehe 20 Oktoba 2012 kama ulivyopangwa.

(f)         Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA)

Kamati ya Uchaguzi ya TFF itakamilisha zoezi la kusikiliza rufaa zilizokatwa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kupitia mchakato mzima  wa uchaguzi wa DRFA, ili kujiridhisha kama matakwa ya Katiba ya DRFA na TFF yamezingatiwa. Kamati ya Uchaguzi itatoa uamuzi kuhusu rufaa zilizowasilishwa kwenye Kamati kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na kuhusu mchakato wa uchaguzi wa DRFA baada ya kikao chake kitakachofanyika Jumanne, tarehe 09 Oktoba 2012.

2.           Kuzingatia Kanuni za Uchaguzi:

(i)  Kamati ya Uchaguzi ya TFF itaishauri Mamlaka husika ya TFF kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi wa Kamati za Utendaji walioko madarakani wanaoingilia michakato ya chaguzi za wanachama wa TFF na kusababisha mikanganyiko katika chaguzi ili ama wandelee kuwa madarakani kinyume na matakwa ya Katiba ya TFF Ibara ya 12(2)(a) au wapitishwe kugombea uongozi kinyume na taratibu zilizowekwa na TFF.

(ii)Kamati ya Uchaguzi ya TFF inasisitiza na kuzitaka Kamati za Uchaguzi za vyama wanachama wa TFF kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF wakati wote wa michakato ya uchaguzi wa viongozi wa vyama hivyo.

Angetile Osiah
KATIBU MKUU
KATIBU- KAMATI YA UCHAGUZI –TFF

No comments:

Post a Comment