TRANSLATE THIS BLOG

Tuesday, September 4, 2012

COAST UNION YAENDA KUJICHIMBIA KAMBINI ZANZIBAR KUJIANDAA NA LIGI KUU

 Baadhi ya wachezaji wa timu ya Coast Union ya jijini Tanga, wakiwa katika Bandari ya jijini Dar es Salaam jana mchana, wakati wakielekea kupanda Boti kwenda Zanzibar kwa ajili ya kuanza kambi yao ya wiki moja kujiandaa na Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayotarajia kuanza Septemba 15, mwaka huu.

 Wakielekea kupanda Boti.



TIMU ya Coast Union ya jijini Tanga imeondoka jana jijini Dar es salaam, kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki moja kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayotarajia kuanza Septemba 15, mwaka huu.


Timu hiyo iliyo chini ya walimu wake, Juma Mgunda na Habib Kondo, leo asubuhi imeanza mazoezi yake katika Viwanja vya Shangani Mnazi Mmoja, ikiwa na wachezaji wake wote.


 Kocha msaidizi wa timu hiyo, Habib Kondo, alisema kuwa wameamua kuweka kambi mjini Unguja ili kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea Ligi Kuu.


Aidha Kondo, alisema kuwa wakiwa mjini Zanzibar ili kufanikisha na kutimiza malengo ya kambi yao timu hiyo itakishirikisha Chama cha Mpira wa Miguu cha Zanzibar ZFA ili kuwasaidia kupata mechi za kirafiki na timu za Visiwani humo.


''Mpaka sasa tayari tumeshapata mechi mbili za kirafiki, ambapo kesho tutashuka dimbani katika uwanja wa Amani, kukipiga na timu ya Falcon, na mechi itakayofuata tutacheza na timu ya Mafunzo,


Kiukweli tunashukuru Mungu tumejitahidi kupata timu nzuri na tumejipanga kufanya vizuri si kushiriki Ligi Kuu tu bali kutetea nafasi nne za juu katika Ligi ya mwaka huu, na ninaamini iwapo hakutakuwa na longo longo na mizengwe ya kubebwabebwa kwa baadhi ya timu basi wasitegemee mtelemko kutoka kwetu, wajiandae kupambana''. alisema Habib


Timu hiyo inatarajia kumaliza kambi yake hiyo ya maandalizi ya Ligi Kuu, Septemba 10, mwaka huu na kurejea jijini Tanga ambako ndiyo Maskani yake makuu.

No comments:

Post a Comment